Hali ya Vyama vya Ushirika Nchini
Vyama vya ushirika vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo kwa karibu miaka 75. Kwa hiyo pamoja na kwamba wamepata matatizo na changamoto nyingi, ni wazi na ni dhahiri kwamba hakuna chombo kingine chochote zaidi ya Ushirika kinachoweza kuwaunganisha wakulima kuwa na sauti moja katika kuendesha shughuli zao za kiuchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla. Vyama vya Ushirika pia vinarahisisha Serikali kupitisha mipango yake ya maendeleo ili iweze kuwafikia wananchi kwa urahisi na uhakika zaidi.
Aidha, baada ya Serikali kuvipa Vyama hivyo fursa ya kushindana na sekta binafsi, Vyama vingi vilishuhudiwa kuingia kwenye mtikisiko wa kiuchumi na baadhi kujikuta kwenye madeni makubwa likiwemo la SHIRECU (1984) LTD. Hata hivyo, Serikali baada ya kuona hivyo ilibadili mwelekeo wake na kuvitaka Vyama Vikuu kuwa wasimamizi na watoa huduma pekee kwa Vyama vya Msingi ili kupanua wigo wa wakulima kupata huduma stahiki, kwa sasa chama kikubwa kinafanya yafuatayo:-
Kufukiza ghala wakati wowote msimu unapofika.
Kuandaa salio na kuzisambaza kwa Vyama vya Msingi.
Kutoa huduma za vitabu.
Kutoa huduma za Elimu ya Uandishi wa Vitabu.
Kuhimiza wakulima kujiunga na vyama vya ushirika vya msingi.
Kusafirisha mbegu za mazao kama pamba, dengu na choroko kwa kutumia magari yake
Kununua Dengu na njegere
Aidha kwa kutoa huduma hizo chama kikuu kimekuwa kikipokea kodi ambazo nazo zimekuwa zikibadilika takribani kila mwaka kutokana na kuongezeka na kupungua hivyo kukifanya chama kishindwe kujiendesha na kuhimili hali iliyopo.
Maendeleo ya Sekta ya Ushirika yanategemea sana dhamira thabiti na yenye tija kwa mustakabali wa maendeleo ya chama kikuu, Vyama vya Msingi na Mkulima kwa ujumla. Tayari Serikali imejipambanua kwa dhamira yake kubwa ya kuimarisha Ushirika. Mambo yanayofanywa na Serikali ni pamoja na kurudisha mali za Ushirika, kuondoa wizi na udanganyifu dhidi ya Wakulima, kuimarisha na hata kubadili mifumo mbalimbali kama vile stakabadhi ghalani. Lengo ni kuviimarisha Vyama vya Ushirika na kuvifanya visonge mbele.