Madhumuni ya Mkutano Mkuu

Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga SHIRECU (1984 LTD) kiliundwa kwa madhumuni yafuatayo kwa mujibu wa Kanuni za Chama kama ifuatavyo:-

1) Kuendeleza hali ya kiuchumi ya wanachama wake kwa kupanga mipango ya kuendeleza shughuli za kilimo cha Pamba na mazao mengine, zinazofanywa na Vyama vilivyojiunga kwa hiari na kwa kuzingatia kanuni na taratibu za Vyama vya Ushirika.

2) Ili kutekeleza malengo yaliyotajwa hapo juu, Chama kitafanya yafuatayo:-

a. Kukuza shughuli za Ushirika kwa wanachama wake na kuhamasisha Vyama vya Msingi katika eneo lake la uendeshaji kujiunga na chama.

b. Kutoa Elimu ya Ushirika na kilimo bora kwa Wanachama, Viongozi na Watendaji wake wa Chama.

c. Kushirikiana na wanachama wake kukusanya, kuhifadhi, na kutafuta masoko ya pamba na mazao mengine kwa lengo la kuwapatia bei nzuri kwa manufaa ya wanachama wake.

d. Kununua na au kukodisha ardhi, majengo, magari, mashine, maghala, ofisi na vifaa mbalimbali kwa matumizi yake na ya wanachama wake.

e. Kununua, kuuza na kusambaza pembejeo za kilimo kwa wanachama wake kwa bei nafuu ili kuboresha kilimo cha pamba na mazao mengine ya kilimo.

f. Kutoa mikopo na misaada ya kifedha kwa wanachama wake kwa mujibu wa masharti hayo, Sheria ya Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015 pamoja na marekebisho na miongozo ya kisheria iliyotolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini.

g. Kuwekeza katika Vyama vingine vya Ushirika vyenye dhima ndogo, taasisi za kibiashara kwa madhumuni ya kuzalisha faida kwa Chama kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015.

h. Kutoa ushauri, mwongozo na usimamizi kwa vyama wanachama katika kuandaa Makadirio ya Mapato na Matumizi.

i. Kufanya mambo mengine halali na ya lazima katika kuendeleza kazi zilizotajwa hapo juu katika kufikia utekelezaji wa malengo ya Chama yaliyoidhinishwa na Mkutano Mkuu na jinsi Sheria ya Vyama vya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 na Kanuni zake za mwaka 2015 inavyoelekeza.

j. Kuongeza thamani ya mazao ya wanachama kabla ya kutafuta masoko kwa ajili yake.